Kuna mambo mawili ambayo kama ukiweza kuyazingatia kuanzia leo basi yatabadilisha kabisa aina ya maisha unayoishi na yatakusaidia kukupa uhakika wa kufanikiwa katika malengo na ndoto ulizonazo maishani mwako.
Moja ni lile ambalo tunajifunza kutokana na maisha ya Anthony Burgess.Alipofikisha miaka 40 Anthony Burgess aligundulika kuwa ana mwaka mmoja tu wa kuishi baada ya madaktari bingwa kugundua kuwa alikuwa na uvimbe mkubwa sana katika ubongo(brain tumor) ambao ulikuwa unazidi kukua kila siku.Mara baada ya kupewa taarifa hii aligundua kuwa hana muda mrefu wa kuishi na mawazo yakaanza kumjia kwani kwa wakati huo alikuwa amefilisika kabisa na hana chochote kile kifedha.Alianza kuwaza jinsi mke wake Lynne atakavyoteseka baada ya yeye kufariki.
Kabla ya kugundulika na tatizo hili Burgess hakuwahi kuwa mwandishi mahiri wa vitabu vya hadithi(novel) lakini siku zote alijua kuwa ana kipaji na uwezo huo ndani yake.Baada ya kutafakari maisha ya mke wake yatakuwaje aliamua kutumia muda wote uliobakia wa mwaka mmoja kabla hajafariki kuandika vitabu ili hata baada ya kufa basi mke wake aendelee kufaidika na mauzo ya vitabu hivyo.Akiwa katika hatua hii hakujua kama vitabu hivyo vitafanikiwa kuuzika lakini hakuwa na chaguo la kufanya kitu kingine.
Burgess anasema “Ilikuwa ni mwezi wa kwanza mwaka 1960” nilipoambiwa rasmi kuwa nina mwaka mmoja tu wa kuishi.Kwa namna isiyo ya kawaida ndani ya mwaka huo mmoja alifanikiwa kuandika vitabu vitano.Cha kushangaza kilichotokea ni kuwa hakufariki kama madaktari walivyotabiri na baada ya hapo alifanikiwa kuandika vitabu zaidi ya 70 kabla hajafariki.
Hili ni jambo la kawaida sana kwa wengi wetu,huwa hatufanyi kitu hadi pale hali inapoonekana haina namna/haina suluhisho lingine.Hii inamanisha kama utalitambua hilo kila siku basi unaweza kufanikiwa kufanya mambo makubwa kila siku.Ubongo wako una nguvu ya kipekee ambayo inaweza kuanza kufanya kazi mara tu utakapotambua kuwa hauna muda wa kutosha.Watu wanaofanikiwa ni wale ambao kila wakati wanajua kuwa muda walionao kufanya mambo ni mchache,kwa sababu hiyo huwa wanajikuta wanaulazimisha ubongo wao kufanya mambo mengi ndani ya muda mfupi.
Kama asingeambiwa kuwa ana mwaka mmoja wa kuishi basi Burgess angekufa na vitabu vyake vyote sabini bila kuviandika.Kuna wengi wataondoka duniani bila kutoa vipaji na uwezo walionao ndani yao,naamini wewe hautakuwa mmoja wa hao watu.Ili leo ichangie katika mafanikio yako ni lazima uiishi kama vile hauna muda wa kutosha-Acha kupoteza muda kwenye mambo yasiyochangia mafanikio yako,acha kuchart mambo yanayopoteza muda wako,acha kusoma vitu vinavyojaza ubongo wako na mambo hasi(negative).
Ili ufanikiwe ni lazima HAMU yako ya mafanikio iwe kubwa kuliko HOFU yako ya kufeli.Siku moja kijana mmoja alimfuata Socrates na akataka amwambie siri ya mafanikio,basi Socrates akamwambia wakutane kesho yake asubuhi mtoni.Asubuhi ilipofika Socrates alimwambia yule kijana waingie ndani ya mto kidogo na ghafla akamchukua na kumtumbukiza kichwa chake ndani ya maji.Akiwa anahangaika kupata hewa Socrates aliendelea kumshikilia kitambo kidogo kisha akamwachia.Baada ya hapo walipotoka nje ya maji Socrates akamuuliza yule kijana-“Wakati nimekuingiza ndani ya maji,ulitamani nini zaidi?” yule kijana akasema-“Hewa”-Socrates akamwambia “kama ukitamani mafanikio kama ulivyohangaika kutafuta hewa wakati uko ndani ya maji basi utafanikiwa,hiyo ndio siri ya mafanikio hakuna siri nyingine ya mafanikio”
Hili ndio jambo la pili unalolihitaji baada ya kuanza kujua kuwa una muda mchache basi lazima uwe na shauku ya mfanikio kama vile unavyokuwa na shauku ya hewa unapokuwa ndani ya maji.Watu wengi huwa wanasema wanataka kufanikiwa lakini ndani kabisa ya mioyo yao shauku yao ya mafanikio bado ni ndogo ukilinganisha na hofu yao ya kufeli.
Utajua kama shauku yako ya mafanikio ni ndogo kama ukifeli mara moja unakata tamaa,utajua kama shauku yako ya mafanikio ni ndogo kama kila siku unasema utaanza kufanya ila hadi leo haujaanza,utajua kama shauku yako ya mafanikio ni ndogo kama maneno ya watu yanakukatisha tamaa kuiishi ndoto yako,utajua kama shauku yako ya mafanikio ni ndogo kama unaweza kuangalia tamthilia kwa lisaa limoja kila siku lakini huwezi kusoma kitabu kwa dakika ishirini kila siku,utajua kama shauku yako ya mafanikio ni ndogo kama unaweza kununua vocha kila wiki ila hauwezi kununua kitabu,jarida,CD ama DVD ya mafunzo fulani.utajua kama hauna shauku ya mafanikio kama unajifunza mambo mengi kila siku lakini hauyafanyii kazi.
Mafanikio katika maisha huwa yanaongozwa na kanuni,kama ukianza leo kuishi kwa kujua kuwa muda wako sio wa kupoteza na pia kuishi kwa shauku ya kiwango cha juu ya mafanikio yako basi sina shaka utafanikiwa.
Kumbuka kuwa Ndoto Yako Inawezekana,
See You At The Top.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni